Match Report: Yanga 4-1JKT Ruvu, Jangwani mwendo mdundo

Na Mwandishi Wetu

yangaphoto

Ushindi huo unaifanya Yanga kuwa katika hali ya utulivu wakati Jumamosi ijayo wakitarajiwa kupambana na wapinzani wao Simba

MSHAMBULIAJI wakimataifa wa Zimbabwe Donald Ngoma ameendekelea kuwa na mwanzo mzuri akiwa na klabu ya Yanga baada ya kufunga bao la kwanza katika ushindi wa mabao 4-1 walioupata leo kwenye mchezo wa Ligi ya Vodacom Tanzania bara.

Hilo linakuwa bao la tatu katika mechi tatu mfululizo alizoichezea timu hiyo iliyomsajili msimu huu akitokea FC Platinum ya kwao Zimbabwe.

Mbali na Ngoma pacha wake Amissi Tambwe naye leo amefikisha idadi ya mabao matatu katika mechi tatu alizoichezea Yanga na kuifanya timu hiyo ikiongoza ligi kwa kufikisha pointi tisa huku wachezaji hao wakiwa vinara wa mabao kila mmoja akiwa na mabao 3.

Ushindi huo unaifanya Yanga kuwa katika hali ya utulivu wakati Jumamosi ijayo wakitarajiwa kupambana na wapinzani wao Simba kwenye mchezo ambao utafanyika kwenye uwanja huo wa taifa Dar es Salaam.

Yanga walianza kwa kasi mchezo wa leo dhidi ya Maafande hao wa JKT Ruvu ambao wanapoteza mchezo wa tatu mfululizo na Ngoma alipoteza nafasi ya wazi baada ya shuti lake kugonga mwamba wa pembeni na kutoka nje.

Kiungo wa kimataifa wa Zimbabwe Thabani Kamusoko aliendelea kungara na katika dakika ya 21, alikosa bao la wazi baada ya mpira wa faulo aliopiga kugonga mwamba wa juu na kutoka nje.

Baada ya kushambulia mfululizo, Yanga walifanikiwa kupata bao la kuongoza katika dakika ya 34 mfungaji akiwa ni Mzimbabwe Dolando Ngoma kwa shuti la mbali akimalizia pasi ya Amiss Tambwe.

Mchezo huo uliendelea kuwa na ushindani mkubwa huku JKT Ruvu inayofundishwa na kocha Fredy Minziro, kuonekana ikipanga vizuri mashambulizi yake lakini washambuliaji Samweli Kamuntu, Sad Kipanga na Mussa Juma walionekana kutokuwa makini.

Katika dakika ya 30 Ngoma, alifunga bao kwa kupokea pasi nzuri ya kisigino kutoka kwa Tambwe na kupiga shuti la mbali lililomshinda kipa wa JKT Ruvu Tony Kavishe.

JKT Ruvu walijitahidi kupambana kuweza kusawazisha bao hilo lakini hadi mwamuzi Anthon Kayombo, anapulizi kipyenga cha mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao hayo mawili.

Kipindi cha pili timu zote ziliunza mchezo huo pasipo kufanya mabadiliko yoyote na iliwachukua dakika mbili Yanga kuandika bao la pili kupitia kwa Tambwe, aliyemalizia mpira uliokuwa umetemwa na kipa Tony Kavishe wa JKT Ruvu kufuatia krosi iliyokuwa imechongwa na Deusi Kaseke.

Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuizindua JKT Ruvu, na dakika ya 49 ilifanya shambulizi la kustukiza na kupata bao moja lililofungwa na beki Michael Aidan, aliyepiga shuti la mbali baada ya kipa wa Yanga Ally Mustapha kutoka golini.

Bao hilo lilionekana kama kuwavuruga Yanga na kuongeza makali ya mashambulizi kwenye lango la JKT Ruvu ambayo nayo ilionwkana kuwa makini baada ya kufanya mabadiliko mara mbili ya kuwaingiza Gaudence Mwaikimba na Abdulrahman Mussa, lakini walijikuta wakipachikwa bao la tatu na Tambwe aliyefunga kwa kichwa dakika ya 62 akiunganisha kona ya Simon Msuva.

Msuva nusura aipatie Yanga bao la nne katika dakika ya 70 baada ya shuti lake akiwa ndani ya eneo la hatari kupanguliwa na kipa wa JKT Ruvu na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kiungo mpya wa Yanga, Thabani Kamusoko aliifungia Yanga bao la nne katika mchezo huo na lakwanza kwake tangu aanze kuichezea timu hiyo akipiga shuti kali lililomshinda kipa Kavishe na mpira kutinga wavinu dakika ya 88.

Kocha Hans van der Pluijm, wa Yanga alionyesha kutoridhishwa na idadi ya mabao na kuamua kumtoa Donald Ngoma, na kumuingiza mshambuliaji Malimi Busungu ambaye naye katika dakika 10 alizocheza alipoteza nafasi mbili za wazi alizozipata baada ya kutengenezewa pasi nzuri na Msuva, pamoja na Geofrey Mwashiuya aliyeingia kuchukua nafasi ya Kaseke.

Kwa matokeo hayo Yanga chini ya kocha Pluijm, imeendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi tisa na inasubiri wapinzani wao Simba ambao kesho watacheza na Kagera Sugar kwenye uwanja huo wa taifa.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *