ALICHOSEMA MASAU BWIRE BAADA YA MCHEZO DHIDI YA AZAM

Simba Makini imekuletea nukuu ya maneno aliyosema msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire baada ya kupokea kichapo cha bao 1 toka kwa Azam kwenye uwanja wa Chamazi hapo Jana.

Washabiki, Wadau na Wapenzi wa Ruvu Shooting, hongereni kwa namna mnavyoisapoti timu yenu kwa hali na mali katika wakati wote, kwa hali yoyote! Mungu azidi kuwabariki, endeleeni na moyo huo, kwa pamoja tutafanikiwa, tutafikia malengo kumaliza msimu huu tukiwa katika nafasi tano za juu.

Poleni kwa matokeo yasiyotarajiwa, tunayoyapata mchezoni, yasiyowiana na uwezo wa kikosi chetu, uwezo wa kikosi chetu ni mkubwa mno lakini ajabu, kiajabu ajabu tunafungwa magoli ya ajabu! Poleni sana, maumivu haya ni ya muda tu, tutakaa sawa kitambo kidogo kijacho.

Ebu tazama mchezo dhidi ya Azam fc, goli walilolipata dakika ya mwisho katika dakika nne za nyongeza, goli la ajabu, goli la “TAMBIKO”!

Wakati mwingine magoli kama haya japo yanaumiza, tusisononeke sana maana, huwa yana sababu zake!

Tulikadiriwa kabla ya mechi kufungwa goli si chini ya tano na hao waliotudhani uwezo wetu ni kidogo katika kucheza mpira lakini, ilifika wakati Azam fc wanaomba dua kwa kuchutama mchutamo usio rasmi kasi ya dakika iongezeke ili mpira umalizike mapema, au litokee kuwezekana walilokuwa wamelikiri kutowezekana (Kupata ushindi) na hilo ndilo lililotlokea, wakapata ushindi kwa goli la “TAMBIKO”

Azam kuthibitisha kweli hicho walichokipata kimekuja tu bila matarajio, waligalagala kwa kushangilia wakitokwa na machozi ya woga kwani hawakuamini na haikuwa rahisi kuamini kwani uwezo wa kuamini hicho kilichotokea muda wa matambiko haukuwepo kwao!

Ruvu Shooting tuko vizuri sana, tutafanya vizuri niaminini kwa asilimia zote! Wana Ruvu Shooting, ondoeni hofu, msiwe na imani haba kama Petro, kuweni na imani ya Ayubu. Ayubu alijaribiwa kwa majaribu kibao, aliteswa, akateseka lakini, MWANAUME hakutetereka, alisimama imara mwisho wa siku akashinda katika yote!

Haya kwetu ni majaribu tu, tupambane nayo kwa wakati wake, tupambane nayo, kwa imani na uwezo wetu, kwa mapenzi ya Mungu, Ruvu Shooting tutashinda!

Muda mfupi ujao, wanaotudharau, kutubeza na kutukejeri, watatusalimia kwa HESHIMA!

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *