Bokungu Awaita Yanga Mezani

BEKI wa kulia wa timu ya Simba Mkongomani Janvier Bokungu ameiita Yanga mezani kama inahitaji huduma yake kufuatia mkataba wake kuelekea ukingoni huku kukiwa hakuna kiongozi yoyote wa timu hiyo aliyemfuata kuhusu kandarasi mpya.

Bokungu ameiambia SIMBA MAKINI kuwa mkataba wake na Wekundu hao utamalizika Agosti 6 lakini mpaka sasa anaona viongozi wa Simba wapo kimya hivyo amezitaka timu zinazohitaji huduma yake kumtafuta ikiwemo Yanga kwakuwa mpira ndio kazi yake.

Beki huyo wazamani wa TP Mazembe alivyotua Simba msimu uliopita alionekana mzito lakini kadiri muda ulivyoenda alizoea mazingira na kugeuka mchezaji muhimu kutokana na uwezo wake wa kucheza pia beki wa kati na kuwasaidia Wekundu hao kutwaa ubingwa wa FA.

“Mkataba wangu umebakiza miezi miwili, nipo tayari kubaki Simba kama watakubali niendelee nao ila kama hawako tayari nitacheza timu nyingine itakayonihitaji hata Yanga au yoyote ile.

“Mimi ni mchezaji na mpira ndio kazi yangu kwahiyo timu yoyote itakayonitaka nipo tayari hata kama ipo nje ya Dar es Salaam nitacheza tu,” alisema Bokungu.

Akizungumzia usajili unaoendelea kufanywa na klabu ya Simba Bokungu alisema ni mzuri ambao utaisaidia kufanya vizuri ndani na michuano ya kimataifa kwavile utaongeza ushindani wa namba ndani ya timu.

Mlinzi Janvier Besala Bokungu katika moja ya purukushani za VPL 16/17

Tayari Simba imemsajili beki Shomari Kapombe kutoka Azam ambaye anatishia nafasi ya Bokungu ndani ya Simba na kukaa kimya kwa viongozi wa klabu hiyo si ishara nzuri kwa Mkongomani huyo.

Bokungu anatarajia kusafiri kesho kuelekea kwao DRC kwa ajili ya mapumziko ya mwezi mmoja na atarejea nchini mwezi Julai.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *