Julio aipa neno Simba baada ya kuiburuza Rayon

KOCHA wa zamani wa timu ya Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ameitaka Simba kutobweteka na ushindi wa bao moja iliyoupata dhidi ya Rayon Sports katika mechi ya kirafiki na badala yake wajipange vizuri kuelekea mchezo wa watani wa jadi Agosti 23.

Julio amesema Simba itafanya kosa kubwa kama itaidharau Yanga katika mchezo wa ngao ya hisani kutokana na kutocheza vizuri katika mechi ya kirafiki dhidi ya Singida United Jumapili iliyopita kitu ambacho kinaweza kuwagharimu siku hiyo.

Kocha huyo amesema mechi ya watani wa jadi siku zote ni ngumu na haitabiriki kwahiyo pamoja na kucheza vizuri dhidi ya Rayon bado si kigezo cha kuwafunga Yanga kama wasipojipanga vizuri na mchezo huo.

John Bocco akiwa chini ya ulinzi wa beki wa Rayon Sports

“Simba imecheza vizuri dhidi ya Rayon leo na Yanga haikucheza vizuri juzi na Singida United ila Simba isijidanganye kuingia kifua mbele kwamba wataibuka na ushindi, mechi ya watani ni ngumu siku zote.

“Yanga ilichelewa kuanza kambi ndio maana wachezaji wake hawakuwa na maelewano mazuri ila hicho si kigezo cha kusema watakuwa hivyo kwenye mechi ya ngao ya hisani dhidi ya Simba,” alisema Julio.

Kichuya alikuwa kwenye kiwango cha juu akiwapa tabu walinzi wenye maumbo makubwa wa Rayon

Mbali na kutoa tahadhari hiyo, Julio amesema wachezaji wa Simba wakikaa kwa muda na kocha Joseph Omog akapata kikosi cha kwanza atakuwa na timu imara kutokana na aina ya wachezaji waliosajiliwa.

“Nimeona Method Mwanjale akicheza na Salim Mbonde kwa mara ya kwanza walicheza vizuri japokuwa kuna kipindi walikuwa wakifanya makosa naamini wakipata muda watacheza vizuri,” alimalizia Julio.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *