KAA CHONJO SAA MBAYA HIZI: SIMBA KUUNGURUMA MKWAKWANI!

Na Mwandishi Wetu
1891872_herol
PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2015/2016, linatarajiwa kufunguliwa leo kwa michezo saba kuchezwa katika viwanja tofauti nchini, huku mchezo mmoja ukitarajiwa kuchezwa kesho.
Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, inatajwa kuwa na msisimko msimu huu kutokana na ongezeko la timu kutoka 14 hadi 16, huku uwepo wa wadhamini ukitajwa kuinogesha ligi.
Katika michezo saba inayochezwa leo, mchezo wa ugenini kwa Simba ambao watacheza na African Sports, ndio unaotajwa kufuatiliwa na wengi, tofauti na michezo mingine sita.
Mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga umekuwa wa msisimko kutokana na Simba kutokupata ushindi kwenye uwanja huo kwa miaka minne sasa.
Mara ya mwisho Simba kupata ushindi kwenye uwanja huo ilikuwa mwaka 2011, walipocheza na Coastal Union na kushinda bao 1-0, bao ambalo lilipachikwa wavuni na kiungo wake (hayati) Patrick Mutesa Mafisango.
African Spotrs, chini ya kocha wao msaidizi Ally Manyani, wametamba kurudisha zama za Mohamed Salim katika miaka ya 1980 katika kikosi hicho.
Manyani alisema, kikosi chake kimejiandaa kufanya vizuri kwenye msimu huu ambao wamepanda tena daraja baada ya kushuka mwaka 1991.
Michezo mingine itakuwa ni Ndanda FC ya Mtwara ambao watakuwa Uwanja wao wa nyumbani Nangwanda Sijaona kuwakaribisha Mgambo Shooting ya Tanga.
Timu hizo ni kati ya timu zilizonusurika kushuka daraja msimu uliopita, lakini ziliweza kufanya vizuri kwenye michezo yao ya mwisho na kuzifanya timu za Ruvu Shooting na Polisi Moro, ziteremke daraja.
Majimaji ‘Wana Lizombe’ ya Songea, ambao wamepanda tena baada ya kushuka mwaka 2010, watawakaribisha Maafande wa JKT Ruvu katika Uwanja wao wa Majimaji, mjini humo.
Washindi wa pili wa ligi hiyo msimu uliopita Azam FC, wenyewe watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons ya Mbeya, katika Uwanja wao wa Chamazi Complex.
Prisons, wataingia kwenye ligi ya msimu huu wakiwa na baadhi ya sura mpya kwenye kikosi chao.
Kocha Salum Mayanga ndio kocha mkuu wa kikosi hicho akichukua nafasi ya Mbwana Makatta, ambaye alishinda tuzo ya kocha bora.
Stand United ‘Chama la Wana’ wakichagizwa na mkataba wao mnono na kampuni ya madini Acacia, watawakaribisha Mtibwa Sugar katika Uwanja wao wa CCM Kambarage, Shinyanga.
Kikosi hicho kimejiimarisha kwa kusajili wachezaji wengi wenye majina na kumchukua kocha Mfaransa Patrick Liewing, aliyewahi kuinoa Simba.
Mtibwa Sugar, imeimarisha kikosi chake kwa kuwarudisha kundini kundi kubwa la nyota wake waliokwenda kujaribu maisha ya soka kwenye timu za Simba na Yanga.
Mchezo mwingine utachezwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ambao utakutanisha timu za Toto Africans ‘Wana kishamapanda’ ambao watakuwa nyumbani kuwakaribisha Mwadui FC ya kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Mchezo huo utaingia kwenye historia msimu huu kutokana na mshambuliaji wa Mwadui FC Jerry Tegete, atakutana na baba yake John Tegete, ambaye ndio kocha msaidizi wa Toto Africans.
Licha ya hivyo vikosi hivyo vina wachezaji wengi wanaofahamiana katika soka la Tanzania.
Mshambuliaji mwingine wa Mwadui FC, Kelvin Sabato ‘Kev Kiduku’ ndio aliibuka mfungaji bora katika kuipandisha timu hiyo bado ni mchezaji wa kuchungwa na mabeki wa Toto Africans wanaongozwa na James Nyakarungu na Hassan Khatib.
Mbeya City ya kocha Juma Mwambusi baada ya kuanza msimu uliopita vibaya, wataanza kibarua chao kwa kucheza na Kagera Sugar katika uwanja wa Sokoine Mbeya.
Mbeya City waliondokewa na kundi lake kubwa la nyota wake imeanza kujijenga upya kwa kuwasajili Juma Kaseja, Haruna Shamte, Gideon Brown, Joseph Mahundi ‘Benteke’ na nyota wengineo.
Kagera Sugar, itaanza msimu bila ya huduma ya nyota wao Rashid Mandawa aliyejiunga na Mwadui FC na Atupele Green aliyemtimkia zake Ndanda FC.
Washambuliaji hao walijenga maelewano makubwa ndani ya uwanja kwa kufunga zaidi 15 msimu uliopita.
Kocha wao Makkata, amefanya usajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi kwa kuwaleta Laurent Mugia, Mtalemwa Mussa na Alhaji Zege, ambao wanacheza safu ya ushambuliaji.
Wiki ya michuano hiyo kwa wiki hii inatarajiwa kufungwa kesho kwa mchezo mmoja wa mabingwa watetezi Yanga ambao watawakaribisha Coastal union ya Tanga, Uwanja Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga wataingia katika mchezo huo wakiwa na rekodi nzuri dhidi ya timu hiyo kwenye mchezo wa mwisho walipokutanaa.
Yanga walipata ushindi wa mabao 8-0, mabao ambayo yanatajwa kuwa mengi tangu ulipoanza mfumo mpya wa ligi kuu.
Coastal Union, ambao watakuwa chini ya kocha wao Mganda Jackson Mayanja wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na rekodoi hiyo ya kufungwa mabao mengi.

Kikosi hicho kimeingia na mchecheto kuhusu mchezo huo na kuwafanya washindwe kuweka wazi lini wanawasili jijini kwa ajili ya mchezo huo.
It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *