KASEJA: Hatuna ‘zali’ na huyu mwamuzi

NAHODHA wa timu ya Kagera Sugar, mlinda mlango Juma Kaseja amebainisha kuwa hawana bahati na mwamuzi Hance Mabena kwani katika mechi mbili alizowachezesha dhidi ya Azam FC wamepokea vipigo vinavyofanana.

Kipa huyo wa zamani wa Moro United, Simba na Yanga alisema mechi ya mwisho ya ligi msimu uliopita walicheza na Azam mwamuzi akiwa Mabena na kujikuta wakiambulia kipigo cha bao moja huku usiku wa jana wakipokea kipigo kama hicho katika uwanja wa Azam Complex.

Juma Kaseja

Kaseja alisema hana maana kuwa mwamuzi huyo ameshindwa kuzitafsiri vizuri sheria 17 za soka katika michezo hiyo ila imekuwa ni kama bahati mbaya kwao katika mechi mbili dhidi ya Azam wamepoteza mwamuzi akiwa huyo huyo na matokeo yakiwa yale yale.

“Hatuna bahati na Mabena, msimu uliopita alituchezesha dhidi ya Azam tukafungwa bao moja na jana tena tumefungwa vile vile, ila sio kama amechezesha vibaya la hasha ni kuwa hatuna bahati nzuri nae,” alisema Kaseja.

Nahodha huyo ambaye pia anatumiwa na timu hiyo kuwanoa makipa wenzake kikosini alielezea jinsi wanavyoumizwa na matokeo waliyopata katika michezo mitatu ya ligi.

Wachezaji wa Azam wakishangilia na kocha wao Aristica Cioba bao lao pekee katika mchezo wa jana

“Matokeo ya mechi tatu za ligi tuliyopata hayaridhishi yanatuumiza ila tunajipanga kuhakikisha tunafanya vyema katika mechi zijazo,” alisema Kaseja.

Kagera imepoteza mechi mbili ambazo ni dhidi ya Mbao FC kwa bao moja nyumbani na jana usiku mbele ya Azam wakati wikiendi iliyopita ikibanwa mbavu na Maafande wa Ruvu Shooting kwa kulazimishwa sare ya bao moja katika uwanja wa Kaitaba.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *