MADEGA: Najua kwanini Bongo haina akina Niyonzima

TANZANIA imeshindwa kupata wachezaji wazuri aina ya Haruna Niyonzima au Emmanuel Okwi katika miaka ya karibuni kutokana na kutoweka umuhimu katika mashindano ya wilaya na mikoa yanayozalisha nyota wengi ambao ni faida kwa Taifa.

Kauli hiyo imetolewa na mgombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Iman Madega ambaye amezindua kampeni zake leo akisema atalipa kipaumbele jambo hilo kwa lengo la kuzalisha wachezaji wazuri ili ligi iwe na ushindani mkubwa.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa klabu ya Yanga, amesema atashirikiana vizuri na vyama vya soka vya Wilaya na Mikoa kwa kuwawezesha fedha ili kuvumbua vipaji na kuwapata akina Niyonzima hapa hapa Tanzania.

Niyonzima kushoto akijadili jambo na kipa Said Mohamed ‘Nduda’

“Ligi yetu inabebwa na wachezaji kutoka nje kwa sababu ligi za wilaya na mikoa hazipewi nafasi, katika uongozi wangu suala hilo nitalifanyia kazi kwa karibu na wachezaji wazuri watapatikana,” alisema Madega.

Madega amesema pia atahakikisha anaisaidia Tanzania kupanda kwenye viwango vya FIFA kutoka kwenye tarakimu tatu hadi kufikia mbili.

“Tupo nafasi ya 120 kwenye viwango vya FIFA, nikiingia madarakani nitajitahidi kushusha hizo tarakimu hadi kufikia nafasi ya 99 na kushuka chini zaidi,” alisema Madega.

Licha ya kuwahi kuwa kiongozi wa juu wa klabu ya Yanga, Madega amesema akiingia madarakani hatakuwa na upendeleo huku akiwatoa hofu mashabiki wa Simba.

Uchaguzi wa TFF utafanyika wikiendi ijayo mkoani Dodoma.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *