Mchezo huo utakuwa wa kwanza kucheza nyumbani kwa Simba inayofundishwa na kocha Dylan Kerr

Na Mwandishi Wetu

kagera

Mchezo huo utakuwa wa kwanza kucheza nyumbani kwa Simba inayofundishwa na kocha Dylan Kerr raia wa uingereza ambaye ameonyesha matumaini makubwa

MABINGWA wa zamani wa Ligi ya Vodacom Tanzania Simba Jumapili ya kesho watakuwa na kibarua kipevu cha kuwakabili Kagera Sugar katika mwendelezo wa Ligi hiyo iliyoanza kutimua vumbi Septemba 12 2015/16.

Mchezo huo utakuwa wa kwanza kucheza nyumbani kwa Simba inayofundishwa na kocha Dylan Kerr raia wa uingereza ambaye ameonyesha matumaini makubwa kwa timu hiyo baada ya kuiongoza kushinda mechi mbili za awali walizocheza ugenini Jijini Tanga na kuvuna pointi sita.

Matokeo hayo yanaufanya mchezo wa kesho kuwa mgumu hasa ukizingatia Kagare Sugar siyo timu nyepesi na imekuwa na rekodi ya kuisumbua Simba zinapokutana uwanja wa taifa watakaocheza hiyo kesho.

Kagera inaingia kwenye mchezo wa kesho ikitoka Ruvuma ilipokubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Majimaji wakati Dylan Kerr na kikosi chake watataka kuonyesha mbinu walizozitumia Tanga na kupata pointi sita ambazo hazikutarajiwa na mashabiki wengi wa timu hiyo hasa mechi na Mgambo JKT.

Makocha wa timu zote mbili wamejinasibu kushinda mchezo huo ambao umebeba dhamana kubwa hasa kwa Simba ambayo wikiendi ijayo itakuwa na mchezo mgumu dhidi ya mahasimu wao Yanga.

Kocha Kerr wa Simba amesema amezungumza na vijana wame na amewaeleza umuhimu wa ushindi kwenye mchezo huo na wamemuhakikishia watashinda.

Nahodha Mussa Hassan ‘Mgosi’ anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya wanamsimbazi huku mshambuliaji wa kiganda mwenye mabao mawili hadi sasa Hamisi Kiiza akitarajiwa kutoa sapoti kwa karibu sawa na Ibrahimu Ajibu.

Kutokana na uzito huo unaokaribiana na ule wa Yanga bila shaka kocha Kerr golini atampanga kipa mzoefu na mkongwe Visent Agbon raia wa Ivory Coast baada ya kukaa benchi mechi mbili za Tanga.

Kwaupande wake kocha Mbwana Makata wa Kagera Sugar, amesema wamekuja Dar es Salaam wakuwa na hasira za kupoteza mchezo wao na Majimaji na watataka kupoza machungu yao kupitia Simba.

Makatta amesema pamoja na kupoteza mchezo huo vijana wake wote wapo katika hali nzuri na hakuna mchezaji wake yeyote ambaye anamuhofia huenda atamkosa kuelekea pambano hilo ambalo linatarajiwa kuwa gumu na lenye ushindani.

Msimu uliopita timu hizo zilipokutana Simba ilifungwa kwa bao moja uwaja wa taifa na katika mechi ya marudiano iliyochezwa Kaitaba Kagera Simba wakalipa kisasi kwa ushindi wa mabao 2-1.

Kocha Makatta katika mchezo wa kesho atakuwa akiwategemea zaidi wachezaji wake Daud Jumanne, Paul Ngwai, George Kavilla na Maregesi Mwangwa ambao wamekuwa mhimili mkubwa kwa timu hiyo baada ya kuondoka kwa Them Felix na kipa Benedict Tinoco.

Kama Simba itashinda itakuwa ni mwanzo mzuri kwa kocha Kerr, kupata ushindi wa tatu mfululizo mbele ya timu ngumu ambazo ziliwashinda makocha waliopita ambao matokeo mabaya yalipelekea kufukuzwa kazi msimu uliopita.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *