Mitambo Yanga bado haijakaa sawa

MITAMBO ya Yanga bado haijakaa vizuri kufuatia kukubali kichapo cha bao moja kutoka kwa maafande wa Ruvu Shooting  katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye uwanja wa Azam Complex, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Wiki iliyopita mabingwa hao waliwafunga Singida United mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliopigwa uwanja wa Taifa ambapo walitokea nyuma na kupata bao la ushindi lililofungwa dakika ya 90 na winga Emmanuel Martin.

Katika michezo hiyo miwili kikosi cha Yanga kimeonekana kukosa muunganiko mzuri hasa kutokea kwenye safu ya kiungo hadi ushambuliaji kutokana na wachezaji wengi kutokuwa pamoja kwa muda mrefu.

Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alijifunga bao hilo dakika ya 21 katika jitihada za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa na Shara Juma upande wa kushoto na kumpoteza malengo mlinda mlango kinda Ramadhan Kabwili.

Kocha George Lwandamina wa Yanga aliwaingiza Maka Edward, Said Juma, Raphael Daud, Juma Abdul na beki raia wa Nigeria Visa Anifoweshe ambao waliongeza kasi na kufanya lango la Ruvu kuwa matatizoni muda mwingi ingawa hawakufanikiwa kupata bao la kusawazisha.

Kijana Maka aliyechukua nafasi ya Said Makapu alicheza vizuri katika nafasi ya kiungo mkabaji ambapo alionyesha uwezo mkubwa wa kupiga mipira mirefu na kupandisha mashambulizi.

Kikosi cha Yanga kitasafiri kesho kuelekea visiwani Zanzibar na jioni kitacheza dhidi ya Mlandege na kuelekea Pemba kuweka kambi kabla ya kukutana na watani wao Simba Agosti 23 katika mchezo wa ngao ya hisani.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *