Mkude Kuisubiri Stars Dar

NAHODHA wa timu ya Simba Jonas Mkude ameondolewa kwenye kikosi cha wachezaji 21 wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kitakachosafari kesho saa 10.45 jioni kuelekea Misri kuweka kambi baada ya kunusurika kifo kwenye ajali ya gari jana.

Mkude hatokuwepo kwenye msafara huo kutokana na ushauri wa madaktari walioelekeza kwamba nyota huyo anatakiwa apate mapumziko ya angalau siku nne ili kuwa fiti.

Nahodha huyo akiwa na wenzake wanne ndani ya gari aina ya Toyota Land cruiser walipata ajali maeneo ya Dumila Morogoro akitokea Dodoma alipoisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa kombe la FA kwa kuifunga Mbao FC mabao 2-1 akiwahi kambi ya timu hiyo.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga ameridhia na kusema kuwa Mkude ataungana na wenzake Juni 8, mwaka huu timu itakaporejea kutoka Misri ambapo hajajaza nafasi ya kiungo huyo ndani ya kikosi chake.

IMG-20170529-WA0030
Jonas Mkude wa pili kushoto akiwa na wachezaji wenzake wa Taifa Stars alipokwenda kuripoti  kambini mchana wa leo kabla hajaruhusiwa kurejea nyumbani

Stars itakuwa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa mwalimu Julius Nyerere kesho saa 7. 45 mchana kwa ajili ya safari hiyo ya kuweka kambi ya siku nane kujindaa na mchezo dhidi ya Lesotho utakaofanyika Juni 10 kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji hao 21 wataungana na wengine wawili ambao ni nahodha Mbwana Samatta na Faridi Mussa wanaocheza ughaibuni katika kikosi hicho na kufanya jumla ya wachezaji kuwa 23 nchini Misri.

Mchezo dhidi Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika nchini Cameroon.

Timu za Uganda na Cape Verde ambazo pia zipo kundi L wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, zitakuwa katika mchezo wa kwanza kuwania nafasi hiyo.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *