Mzee Kilomoni alimwaga mboga, watu wamemwaga ugali

ULE msemo wa “ukimwaga mboga tunamwaga ugali”¬†umethibitishwa leo baada ya wanachama wa klabu ya Simba kupitia mkutano mkuu kumtoa katika orodha ya wadhamini Mzee Hamis Kilomoni kufuatia kupeleka kesi katika Mahakama za kawaida kinyume na katiba ya Simba ibara ya 51.

Alhamisi iliyopita Mzee Kilomoni aliweka zuio katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili mkutano wa leo usifanyike kutokana na viongozi wakuu wa klabu hiyo Rais Evans Aveva na Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kushikiliwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za utakatishaji fedha.

Kaimu Rais wa klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amewaongoza wanachama kufikia maamuzi hayo katika mkutano mkuu uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere International Conference Center.

“Mzee Kilomoni amevunja katiba ya Simba ibara ya 51, katiba ya TFF, CAF na FIFA kwa kupeleka kesi katika mahakama za kawaida hivyo Kamati ya Utendaji imemtoa kwenye nafasi ya udhamini na kwakua nyinyi wanachama ambao ndio wamiliki wa klabu mmeridhia jambo hili limepitishwa rasmi,” alisema Try Again.

Mkutano huo pia umemsimamisha uanachama Mzee Kilomoni na umemtaka kwenda kufuta kesi hiyo na akishindwa kufanya hivyo atafutiwa uanachama wake moja kwa moja.

Adam Mgoyi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ameteuliwa kuwa mdhamini mpya wa klabu hiyo kuziba nafasi ya Mzee Kilomoni.

Wakati huo huo Mkutano huo umemthibitisha Juma Kapuya kuwa mdhamini wa klabu hiyo kuchukua nafasi ya Ally Sykes aliyefariki dunia miaka kadhaa iliyopita.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *