Okwi ‘azindua’ tuzo za Vodacom

MSHAMBULIAJI wa Simba Emmanuel Okwi amekuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018 baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa mwezi Agosti.

Okwi ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili Mohamed Issa wa Mtibwa Sugar na Boniface Maganga wa Mbao FC waliopendekezwa na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyoketi jana Jumatano.

Ushindi wa Okwi unatokana na kutoa mchango mkubwa katika mchezo wa Simba dhidi ya Ruvu Shooting uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 7-0, huku yeye akifunga mabao manne. 

Pia Okwi amekuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga hat trick  (mabao matatu katika mchezo mmoja) katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoshirikisha timu 16, ambapo aliifunga ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Mwezi huo ulikuwa na raundi moja tu iliyochezwa Agosti 26 na 27 mwaka huu ambapo kila timu ilicheza mechi moja. 

Kutokana na kutwaa tuzo hiyo, Okwi ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ atazawadiwa kitita cha Sh. 1,000,000 (milioni moja) na Kampuni ya Vodacom Tanzania ambayo ndio wadhamini wakuu wa ligi.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *