Omog aonyesha ‘utajiri’ wake

KOCHA Joseph Omog ameonyesha upana wa kikosi chake baada ya kutumia wachezaji wengi wa akiba na kushinda mabao 5-0 dhidi ya Hard Rock ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Uhuru.

Katika mchezo huo Omog alimtumia kiungo James Kotei pekee ambaye ndiye anapata nafasi katika kikosi cha kwanza huku wachezaji 10 waliobaki wakiwa ni wale wanaotokea benchi.

Nyota wa kikosi cha kwanza kama Haruna Niyonzima, John Bocco, Salim Mbonde, Mzamiru Yassin na Erasto Nyoni walikuwa jukwaani kushuhudia wenzao wakifanya mauaji hayo.

Mwinyi Kazimoto akimtoka mlinzi wa Hard Rock

Simba imefunga mabao 12 ndani ya wiki moja kufuatia ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hali inayoonyesha msimu huu wamepania kufanya vizuri.

Kiungo Mohammed Ibrahim aliifungia Simba mabao mawili kipindi cha kwanza huku akisaidia kupatikana kwa bao moja katika mchezo huo.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Nicholas Gyan, Said Ndemla na Mwinyi Kazimoto kipindi cha pili.

Simba itakutana na Azam FC katika mchezo ujao wa ligi kuu utakaofanyika katika uwanja huo huo wa Uhuru.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *