SIMBA: Hii ni Mechi ya Kisasi

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema mchezo wa kesho wa nusu fainali dhidi ya Azam FC utakuwa ni wa kulipa kisasi baada ya kukubali vichapo viwili katika michezo iliyopita mbele ya Wanalambalamba hao.

Simba ina kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa ligi kwenye mzunguko wa pili kwa bao moja dhidi ya Azam na matokeo kama hayo katika fainali ya michuano ya Mapinduzi iliyomalizika mwezi Januari visiwani Zanzibar na sasa wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

Makamu wa Rais wa klabu hiyo Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema wachezaji pamoja na benchi la ufundi wamejipanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo kwa kulipa kisasi kwa Azam pamoja ili watinge fainali ya michuano hiyo na hatimaye kunyakua ubingwa.

“Azam wametufunga katika michezo miwili tuliyokutana nao katika siku za karibuni, hatuwezi kukubali kufungwa mara tatu mfululizo na timu moja. Pia michuano hii tunaichukulia kwa uzito mkubwa kwani tunataka kunyakua taji,” alisema Kaburu.

Kaburu alisema pia kikosi cha timu hiyo tayari kimewasili jijini Dar es salaam kikitokea mkoani Morogoro kilipokuwa kimeweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo huku wachezaji wakiwa na morali ya hali ya juu.

“Kikosi kimewasili jijini leo, maandalizi ya mchezo yamekamilika na kocha Joseph Omog pamoja na benchi lake la ufundi wameridhika na kambi wakiwa wanasubiri muda ufike kwa ajili ya mchezo huo.”

Jumapili kutakuwa na mchezo mwingine wa nusu fainali ya pili kati ya Mbao FC dhidi ya Yanga utakaofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *