Simba kimeeleweka, mabadiliko yapita kwa kishindo

HATIMAYE wanachama wa klabu ya Simba wameandika historia mpya kwa kupitisha kwa kauli moja mfumo wa uendashaji klabu hiyo ambapo sasa utaendeshwa kwa hisa, maamuzi hayo yakifikiwa katika mkutano mkuu uliofanyika ukumbi wa Mwalimu Nyerere International Conference center.

Mfumo huo unamfanya mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’ ambaye alionyesha nia ya kuwekeza hisa za asilimia 51 zenye thamani ya sh bilioni 20 kukaa tayari ingawa ataruhusiwa kununua asilimia 50 pekee huku nyingine zikibaki kwa wanachama.

Kaimu Rais wa klabu hiyo Salim Abdallah ‘Try Again’ amewashukuru wanachama wa klabu hiyo waliojitokeza na kukubali kwa moyo mkunjufu kupitisha muundo huo ambao utakuwa na faida kwa wanachama na mashabiki wote.

“Leo kamati yangu ya utendaji italala usingizi mnono kutokana na jambo kubwa na la kihistoria kwa klabu yetu ambalo tumelifanya hii leo Agosti 20,” alisema Try Again.

Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Kamati ya utendaji itatengeneza kanuni na kuunda kamati huru ili kuandaa tenda kwa mujibu wa taratibu za ununuzi wa hisa na kuzichambua hadi apatikane mmoja.

Baada ya hatua zote kukamilika ikiwemo nyaraka zote, kutaitishwa tena mkutano mkuu wa wanachama kwa ajili ya kutangaza makubaliano hayo na kuzindua rasmi mfumo huo.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *