Simba yapata pointi moja Okwi akiwa jukwaani

TIMU ya Simba imeshindwa kupata bao bila mshambuliaji wake nyota Emmanuel Okwi katika mchezo wa pili wa ligi kuu dhidi ya Azam FC mtanange uliofanyika kwenye uwanja Azam Complex nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Hiyo ni mechi ya kwanza ya ligi kwa Simba kucheza katika uwanja huo tangu bodi ya ligi iidhinishe kutumika kwa mechi zinazohusisha timu za Simba na Yanga wiki iliyopita.

Okwi alifunga mabao manne katika ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa kwanza wa ligi Agosti 26 lakini akiwa jukwaani baada ya kuchelewa kuwasili nchini akitokea Misri, ameishuhudia Simba ikishindwa kupata bao.

Okwi amewasili nchini mchana wa leo akitokea Uganda sambamba na beki Juuko Murshid waliokuwa katika majukumu ya timu yao ya taifa ‘The Cranes’ ambao walikuwepo katika uwanja wa Azam Complex kuwatazama wenzao.

Kocha Joseph Omog aliwatumia John Bocco na Nicholas Gyan katika safu ya ushambuliaji huku Haruna Niyonzima na Shiza Kichuya wakicheza pembeni lakini walishindwa kupata bao lolote.

Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo hasa kipindi cha kwanza kwa kufika zaidi langoni kwa Azam lakini hawakuwa na madhara kwa mlinda mlango Razack Abalora.

Kocha wa Azam Aristica Cioba alimuingiza kiungo Frank Domayo kuchukua nafasi ya Enock Agyei ambaye aliimarisha safu ya kiungo iliyokuwa imemilikiwa na Mzamiru Yassin na James Kotei.

Timu zote zimefikisha pointi nne baada ya mechi mbili ambapo Azam ilishinda mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Ndanda FC.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *