SportPesa yaupa jukumu zito uongozi wa Yanga

KAMPUNI ya SportPesa ambayo ni wadhamini wa klabu ya Yanga imeutaka uongozi wa mabingwa hao kudhibiti uuzwaji holela wa vifaa vya michezo vyenye nembo yao ili kujipatia mapato na kujiendesha kisasa kama ilivyo duniani kote.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo nchini, Tarimba Abbas ameyasema hayo katika makabidhiano ya vifaa vya michezo kama jezi, viatu, jezi za mazoezi mipira kwa ajili ya kuzitumia katika michuano mbalimbali kuanzia msimu huu.

Tarimba amesema kuwa kuna watu wanafaidika na mauzo ya jezi hizo huku klabu ikiwa haifaidiki chochote kitu ambacho hakipaswi kuonekana kuanzia msimu ujao.

“Ukienda mtaani utakuta kuna watu wanauza jezi za Yanga, kibaya zaidi kuna hata za wachezaji wapya akiwemo Ibrahim Ajib huku Yanga wakiambulia patupu. Hilo suala halipaswi kuonekana,” alisema Tarimba.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya utendaji ya klabu ya Yanga, Salum Mkemi amesema watashirikiana na jeshi la Polisi, Shirika la viwango (TBS) na Tume ya ushindani ili kudhibiti uuzwaji huo holela.

“Kwa sasa tumejipanga kuhakikisha vifaa vyote vyenye nembo ya Yanga haviuzwi bila klabu kupata mapato. Tutaweka mawakala maalum wenye vitambulisho kwa ajili ya uuzaji wa vifaa hivyo,” alisema Mkemi.

Yanga itaanza kutumia vifaa hivyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United muda mfupi kutoka sasa.

It's only fair to share...Share on FacebookShare on Google+Tweet about this on TwitterShare on LinkedIn

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *